Je, Unatumia viuatilifu kwa usahihi? SUA na TPHPA wana jibu

Ikiwa ni muendelezo wa kutengeneza wahitimu wenye weledi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeshirikiana na Mamlaka ya Afya ya mimea na Viuatilifu (TPHPA) kutoa mafunzo kwa wanafunzi wake.

Baadhi ya aina tofauti za teknolojia ya vinyunyizi vinavyotumika Tanzania

Wanafunzi hao ambao ni shahada ya kwanza na wengine shahada za uzamivu wamepewa mafunzo kwa vitendo kuhusiana na aina tofauti za teknolojia za vinyunyizi zinazotumika nchini.

Suala la mavazi kinga lilitiliwa mkazo ambapo mwezeshaji alisisitiza kuwa ni muhimu kuvaa mavazi sahihi kulingana na kiuatilifu husika.

Bwana. Christian Mayige, TPHPA akieleza umuhimu wa kutumia mavazi kinga

“Wakulima wengi hudhani mavazi kinga yote ni sawa, hili lina ukweli lakini si kwa asilimia zote. Baadhi ya viuatilifu huhitaji mavazi kinga mahsusi kulingana na aina ya viambata amalifu vilivyopo. Mfano kuna viuatilifu ambavyo sumu yake huweza kupenya hivyo barakoa zinazotumika ni tofauti. Hakikisha unajua vizuri aina ya kiuatilifu unachotumia ili kuchagua barakoa au mavazikinga yaliyo sahihi” ~ Christian Mayige, Afisa Kilimo TPHPA

Bw. Christian Mayige, TPHPA akionesha aina tofauti za barakoa kulingana na aina za viuatilifu

Akifundisha kuhusu matumizi ya vinyunyizi (sprayers), alisema kuwa kwa Sasa teknolojia imeendelea na kuna vinyunyizi vinavyoendeshwa kwa Umeme/betri/Mafuta na hivyo kurahisisha kazi ya mkulima.

Kelvin Lava, mwanafunzi CPM mwaka wa pili akionyesha matumizi ya kinyunyizi cha umeme

Washiriki walijifunza jinsi ya kunyunyuzia viuatilifu na kujua kiwango gani watumie katika eneo gani.

Bw. Erasto, TPHPA akionesha namna ya kunyunyuzia eneo dogo la majaribio ili kujua kiwango cha kiuatilifu cha kutumia katika eneo husika.

“Ni muhimu kuangalia spidi/mwendo wakati unanyunyuzia kiuatilifu, hakikisha unapiga kwa usahihi kulingana na zao husika. Mfano, unyunyuziaji kwenye mazao yenye kimo kirefu hutofautiana na mazao mafupi. Aina ya nozeli pia hutofautiana kulingana na aina ya kisumbufu, hivyo ni muhimu kujiridhisha na usifanye kwa mazoea” ~ James Simon, TPHPA

Bw. James, TPHPA akifundisha kuhusu aina mbalimbali za vinyunyizi na matumizi ya nozeli sahihi

Wakionyesha kuelewa na kufurahia somo, washiriki hawakukosa maswali,

“Kuna wakati nilifuata maelekezo sahihi ya kwenye Kibandiko na nikanyunguzia kiuatilifu kulingana na maelekezo pamoja na kutumia kiwango sahihi, lakini niliporudi shambani baada ya muda nikakuta bado wadudu wapo Kama kwamba hapakupigwa kiuatilifu, nini sababu?” ~ Kennedy Vitus, mwanafunzi shahada ya uzamili, Teknolojia ya mbegu

Akijibu swali hilo, Prof. Gration Rwegasira ambaye pia ni mkufunzi wa somo, alisema: “Ni muhimu kujua aina ya mdudu na hatua yake ya ukuaji, baadhi ya wadudu hudhibitiwa kwa kutumia viuatilifu aina tofauti tofauti kulingana na hatua ya ukuaji.

Lakini pia baadhi ya wakulima wamekuwa wakichanganya viuatilifu, hali hii hupunguza uwezo wa kufanya kazi kwa viuatilifu.  Pengine muda wa matumizi wa kiuatilifu Unaweza kuwa ulikuwa umepita.

Aliongeza kuwa hizi ni baadhi ya sababu ambazo hupelekea kiuatilifu kisifanye kazi. Hivyo ni muhimu kujiridhisha na kila kitu kabla ya kuamua aina gani ya kiuatilifu kitumike.

Prof. Gration Rwegasira, SUA akiwaelekeza jambo wanafunzi

Naye Dr. Yasinta Nzogela aliwahimiza wanafunzi kuhakikisha kuwa wanajifunza kwa usahihi na kufanya kwa vitendo ili waweze kuwa na maarifa toshelevu ya kuwahudumia wakulima na hata mashamba yao wenyewe.

Wanafunzi walionyesha kuridhishwa na mafunzo hayo na kuomba kuwa kuwe na mwendelezo hata kwa miaka mingine.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa sababu hiki ndicho tutaenda kukifanya shambani, ni muhimu kwa kuwa tutaweza kuwaelekeza wakulima kwa usahihi zaidi” ~ Rehema Chiyumbe, mwanafunzi Shahada ya Uzamili ya Teknolojia ya Mbegu.

Rehema Chiyumbe, Mwanafunzi shahada ya uzamili ya Teknolojia ya mbegu
Dramani Londjiringa, mwanafunzi wa shahada ya uzamili SUA kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya CONGO akionesha matumizi ya kinyunyizi aina ya “mist and dust blower” 
Gladness Mhelwa, mwanafunzi CPM mwaka wa pili akionesha matumizi ya kinyunyizi
Picha ya pamoja baada ya mafunzo

Related Posts