Wanafunzi wa SUA wapatiwa mafunzo kuhusiana na Teknolojia za unyunyuziaji wa viuatilifu.

Wanafunzi wanaosoma shahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa mazao (CPM) mwaka wa pili pamoja na wanafunzi wa shahada za uzamili Kutoka Idara ya Mimea vipando na Mazao ya Bustani wamepatiwa mafunzo juu ya Teknolojia za unyunyuziaji wa viuatilifu.

 

Mafunzo hayo yametolewa kwa kushirikiana na mamlaka ya Afya ya mimea na viuatilifu (TPHPA) ambapo wanafunzi hao wamejifunza kuhusu mchanganyiko wa viuatilifu, aina za viuatilifu, matumizi sahihi ya viuatilifu, kusoma na kuelewa vibandiko vinavyowekwa katika viuatilifu, madhara yatokanayo na matumizi mabovu ya viuatilifu pamoja na nini cha kufanya ili kupunguza na ikiwezekana kuepuka madhara hayo.

Ndugu. James Simon kutoka TPHPA akitoa mafunzo

“Matumizi sahihi ya viuatilifu na vifaa vinavyotumika kunyunyuzia ni muhimu, tumewaelekeza pia kuhusu mabomba ya unyunyuziaji na yanavyofanya kazi. Mfano, endapo mkulima anataka kuua magugu na akatumia nozeli ambayo inatumika kunyunyuzia viuatilifu vya wadudu au magonjwa hataweza kupata matokeo chanya.” ~ James Simon, TPHPA

Ameongeza kuwa lengo hasa la TPHPA ni kuhakikisha kuwa jamii inafahamu matumizi sahihi ya viuatilifu na kupunguza matumizi holela ili kuongeza uzalishaji na kupunguza madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi.

“Imekuwa ni fursa nzuri sana kukutana na wanafunzi ili kuendelea kuwajengea uwezo kuhusiana na matumizi ya viuatilifu. Watumiaji wengi hawafuati matumizi sahihi, hivyo fursa hii itasaidia wanafunzi Hawa kuwa mabalozi wazuri.” ~ Christian Mayinge, Afisa Kilimo TPHPA

“Kwa Sasa Chuo kinaunganisha tasnia ya Elimu na tasnia ya viwanda, na katika hilo tuliwaalika TPHPA na wamekuja kuongezea pale ambapo sisi tumefanya. Hii itawasaidia wanafunzi wetu kuongeza maarifa zaidi na kuwa na msaada kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu.” ~Dr. Yasinta Nzogela, Mhadhiri  SUA

Dr. Yasinta Nzogela (mbele) pamoja na washiriki wa mafunzo

Washiriki wa mafunzo hayo wameonyesha mwitikio chanya na namna mafunzo haya yalivyo muhimu.

“Nimeongeza ujuzi kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu, nimefahamu kuwa TPHPA inaruhusu watu wengine kuweza kutengeneza viuatilifu na imenihamasisha kufanya tafiti kuhusiana na kutengeneza viuatilifu asilia kwa udhibiti wa visumbufu.” ~ Fatma Hassan, shahada ya Uzamili

“Nawashauri wakulima kuhakikisha wanasoma maelekezo kwenye vibandiko na kuyafuata kwa usahihi, na pia kuhakikisha wanavaa mavazi kinga wakati wa unyunyuziaji viuatilifu ili kulinda afya zao” ~ Ngusa Ngusa (mwanafunzi shahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa mazao)

wawezeshaji kutoka TPHPA pamoja na mhadhiri kutoka SUA

Wanafunzi hao wataendelea na mafunzo yao kwa siku ya pili ambapo watafanya kwa vitendo yale yote ambayo wamejifunza. Tunawashukuru TPHPA kwa kuendelea kushirikiana na SUA kwa karibu, SUA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi katika kutoa mafunzo na kuwajengea wanafunzi uwezo ili kupata wahitimu bora watakaotatua changamoto za jamii.

Related Posts