Utunzaji wa mazingira katika zahanati ya Uwanja wa Taifa, Morogoro

Siku ya tarehe 07/06/2024 Asasi ya Maendeleo ya Jamii (Community Development Association – CDA) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ilifanya tukio la utunzaji wa mazingira katika zahanati ya Uwanja wa Taifa, Morogoro. Shughuli hiyo ilijumuisha ufanyaji usafi, upandaji miti, na ugawaji wa vifaa vya usafi.

Afisa Mtendaji wa Kata ya uwanja wa taifa Bi. Chausiku, akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, alitoa shukrani zake kwa kusema:

“Kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Asasi ya Maendeleo ya Jamii (CDA) kutoka SUA kwa juhudi zenu kubwa za kuimarisha mazingira yetu. Kitendo hiki kinaonesha jinsi gani tunavyoweza kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha tunakuwa na mazingira safi na salama kwa afya zetu. Tunathamini sana mchango wenu.”

Mwenyekiti wa CDA, Ndg. Ndege Magoma, pia alitoa neno la shukrani kwa Uongozi wa Kata na Zahanati, akisema:

“Napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Uongozi wa Kata na Zahanati kwa ushirikiano wenu mzuri katika tukio hili. Lengo letu kama CDA ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira na huduma za afya. Tunaamini kwa kushirikiana, tutafanikiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu. Shughuli hizi zinaonesha dhamira yetu ya dhati ya kuhakikisha tunakuwa na mazingira bora kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.”

Tukio hilo limeleta faida nyingi kwa jamii, kama vile kuboresha afya kwa kufanya usafi na kupanda miti, ambapo mazingira yanakuwa safi na salama hivyo kupunguza magonjwa yanayotokana na uchafu. Pia, limeimarisha ushirikiano kati ya wanajamii, asasi, na serikali katika kutunza mazingira. Ugawaji wa vifaa vya usafi umetoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa usafi na jinsi ya kudumisha mazingira safi. Kwa ujumla, tukio hili limekuwa na mafanikio makubwa na limeleta mwamko wa umuhimu wa kutunza mazingira kwa wanajamii wa Morogoro.

 

Share this

Related Posts