WANANCHI WATAKIWA KUNUNUA MICHE YA MATUNDA KUTOKA SUA

Wananchi wametakiwa kununua miche ya matunda mbalimbali kutoka kwenye vyanzo vya uhakika kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho kina vyanzo vizuri vya kupata malighafi za kuzalisha miche kutoka kwenye mashamba yanayotumika kwa ajili ya kupata vikonyo vya kuzalisha miche ya aina tofauti.

 

Meneja wa Shamba la Bustani katika Idara ya Shamba la Mafunzo la SUA Bw. Roman Mfinanga (kushoto) akiwa na mteja wa miche ya miembe katika banda la SUA. Picha na Asifiwe Mbembela.

Akizungumza na SUAMEDIA Julai 20, 2023 katika Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam Meneja wa Shamba la Bustani katika Idara ya Shamba la Mafunzo la SUA Bw. Roman Mfinanga amesema miche shina inayotumiwa na SUA katika uzalishaji ni ile ambayo inamethibitika kufanya vizuri nchini.

“Mwananchi akifika hapa kwenye banda la SUA ana uhakika wa kupata miche bora ambayo itampatia matunda yaliyo bora na itakuwa inadumu kwa muda mrefu kwenye shamba lake kwa ubora ule ule”, amesema Bw. Mfinanga.

Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa miche ya matunda bora yanayoweza kuhimili mabadiliko hayo ili upatikanaji wa matunda kama sehemu ya chakula uwe wa uhakika na ubora ambapo Kitengo cha Bustani kimeendelea kuimarisha uzalishaji wa miche bora ambayo wananchi wanaweza kupata miche mizuri katika kitalu cha Chuo itakayowawezesha kupata chakula pamoja na kipato cha ziada.

Aidha Bw. Mfinanga amezitaja shughuli zinazofanywa na Kitengo hicho cha Bustani kuwa ni uzalishaji wa miche ya matunda, mboga na viungo vya aina tofauti pamoja na mimea ya mapambo ambapo shughuli hizo hufanywa kwa vitendo na wanafunzi wanaosoma Shahada za Awali na wananchi wengine wanaofika SUA kwa ajili ya kujipatia mafunzo mbalimbali yanayohusiana na uzalishaji bora wa mazao ya kilimo cha bustani.

Mawasiliano: 0766646733

0743677370

 

 

Related Posts