Wakulima na wafugaji wa samaki wametakiwa kufika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kujipatia mbegu bora za vifaranga vya samaki kwa kuwa mbegu zinazotumika katika uzalishaji wa vifaranga hivyo ni za uhakika.
Wito huo umetolewa Agosti 4, 2023 na Afisa Mafunzo wa Kitengo hicho Bi. Stella Genge wakati akizungumza katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere mjini Morogoro.
Bi. Stella amesema wanazalisha vifaranga vya kutosha kwani kwa sasa wana uwezo wa kuzalisha vifaranga 134,400 kwa mwezi kwa kutumia mtambo ambao unabeba majagi sita ya kutotoreshea.
“Kwa hiyo wasisite kuja SUA, waje wajipatie vifaranga vingi na sio tu vifaranga vingi lakini vilivyo bora ambavyo haviwezi kukusumbua, vifaranga hivi vya samaki vinakuwa vizuri sana na vina uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa kwa sababu tuna mbegu ambazo ni nzuri zaidi”, amesema Bi.Stella.
Afisa Mafunzo huyo amesema kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa wafugaji kwamba vifaranga havikui hii ni kutokana na sababu ya kununua vifaranga kutoka kwenye vyanzo visivyoeleweka ambavyo vinauza vifaranga visivyokuwa na ubora na matokeo yake wafugaji kupata hasara.
“Kwa nini nasema waje SUA ni kwa sababu tuna utaalamu wa kutosha katika suala la uzalishaji wa vifaranga, mfugaji hana sababu ya kujiuliza kwa sasa aende wapi akape vifaranga kwani unaponunua vifaranga kutoka SUA unakuwa na uhakika wa kupata vifaranga bora vinavyokuwa kwa haraka na havitakusumbua katika mabwawa yako”, amesisitiza Bi. Stella.
Akizungumzia mwitikio katika ufugaji wa samaki kwenye mabwawa Bi. Stella amesema kwa sababu tasnia ya ufugaji wa samaki ni changa na bado inaendelea kukua watu wanaitikia kwa taratibu lakini wana imani kuwa hapo baadaye baada ya wafugaji kuwa na elimu ya kutosha basi tasnia hiyo itakuwa ni chanzo kikubwa cha ajira.
Kama nilivyosema hii tasnia ya ufugaji samaki ni changa watu wengi hawana elimu kwa hiyo kwanza tunampa elimu mfugaji kuanzia namna ya kuchagua eneo linalofaa kwa ajili ya mabwawa, ujengaji wa mabwawa yenyewe, vifaranga bora vikoje, utotoreshaji wake, ulishaji hadi kufikia samaki mkubwa wa kumpeleka sokoni, tunatoa full package na mteja akishanunua vifaranga kwetu tunaendelea kumpa ushauri bure pindi samaki wake wanapopata changamoto yoyote”, amesema Bi. Stella.
Mawasiliano
Simu:0766646733
0743677370