FAHAMU KILIMO CHA MIGAZI (MICHIKICHI)

FAHAMU KILIMO CHA MIGAZI (MICHIKICHI) KUTOKA SHAMBA LA MFANO LA MAFUNZO SUA

Migazi au Michikichi ni mimea ya aina ya mitende inayostawi vizuri katika udongo wenye rutuba nyingi na usiojaa maji kila wakati. Mimea hii pia hupendelea mvua nyingi. Matunda ya Migazi au Michikichi hutengeneza mafuta yanayoitwa mawese.
Aina za Migazi
Kuna aina kuu tatu za Migazi. Kwanza ni Dura, ambayo ina mbegu kubwa iliyozungukwa na nyama nyembamba. Aina hii hutoa mafuta kidogo ikilinganishwa na nyingine. Pili ni Tenera, ambayo ina mbegu ndogo iliyozungukwa na nyama nyingi, na hivyo hutoa mafuta mengi. Aina ya tatu ni chotara wa Dura na Tenera, ambayo hutoa mafuta kiasi.
Shamba la Mfano la Mafunzo SUA lina Migazi aina ya Tenera, ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha motisha katika mchakato wa kujifunza.
Ukuzaji wa Migazi na Hatua zake
Migazi inaweza kukuzwa kwa kupandikiza kwenye kitalu au moja kwa moja shambani. Kupandikiza kwenye kitalu, mbegu za Migazi hupandwa kwanza kwenye kitalu. Matuta katika kitalu yanakuwa na upana wa mita moja (1) na urefu wowote kulingana na hali ya ardhi.. Mbegu hupandwa kwenye mistari iliyoachwa kati ya mche na mstari kwa umbali wa sentimita 45 hadi 60. Miche huchukua wiki tatu hadi nne kuchipua. Miche huhamishiwa shambani ikiwa na urefu wa sentimita 25 hadi 30.

 

Hatua Muhimu za Kuzingatia Wakati wa Upandaji
Ondoa magugu yote na safisha shamba. Jenga mashimo yenye kina cha sentimita 60 na upana wa sentimita 60. Tenga udongo wa juu na wa chini wakati wa kuchimba mashimo. Changanya udongo wa juu na samadi au mboji kwa uwiano wa debe moja kwa moja, kisha rudisha shimoni. Hakikisha kuwa shimo lina udongo uliochanganywa na samadi.
Mbolea na Urutubishaji wa Udongo
Migazi inakuzwa kwa kutumia mbolea ya chumvi chumvi kwa muda wa miaka miwili hadi mitatu. Pia, matumizi ya mboji ni muhimu kudumisha rutuba na afya ya udongo na mimea kwa ujumla.
Magonjwa na Wadudu Waharibifu
Migazi mara nyingi huathiriwa na magonjwa na wadudu waharibifu, kama vile mchwa. Mbinu mbalimbali hutumiwa kuzuia na kutibu mashambulizi haya, kama vile kupuliza dawa ya kuua mchwa au kuloweka mizizi kabla ya kupanda ili kupunguza mashambulizi.
Mazingatio katika Kuvuna na Kuhifadhi
Migazi huanza kuzalisha matunda yake baada ya miaka 3-4, kulingana na aina na mazingira ya upandaji. Mgazi mmoja unaweza kutoa kati ya mikungu 8-9 kwa mwaka yenye uzito kati ya kilo 40 mpaka 50. Mti mmoja wa Mgazi unaweza kutoa lita 40.5 za mafuta ya mawese kwa mwaka. Matunda ya Mgazi yanapokomaa, yanapaswa kuvunwa na kuchakatwa kulingana na maelekezo ya wataalamu.
Imeandaliwa na:
Idara ya Shamba la Mfano la Mafunzo | Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo – SUA | 0766737453

Related Posts