Fika banda la SUA ujionee Maabara inayotembea maalum kwa utotoreshaji wa vifaranga vya Samaki

Chuo Kikuu cha Sokoine chaKilimo (SUA) kupitia Kitengo cha Ukuzaji wa Viumbe Maji kilichopo Idara ya Shamba la Mafunzo kwa mara ya kwanza katika Maonesho ya Nanenane kimekuja na Maabara inayotembea maalum kwa ajili ya utotoreshaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato.

Maabara inayotembea maalum kwa ajili ya utotoreshaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato ikiwa kwenye Maonesho ya Nanenane banda la SUA

Hayo yamebainishwa Agosti 4, 2023 na Afisa Mafunzo wa Kitengo hicho Bi. Stella Genge wakati akizungumza  katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere mjini Morogoro.

Bi.Stella amesema lengo ya kupeleka Maabara hiyo kwenye maonesho ya Nanenane ni kutaka kukidhi kiu ya wakulima ambao kwa muda mrefu walikuwa na hamu ya kuona namna vifaranga vya samaki vinavyozalishwa.

“Tumeona sasa tuje na Maabara hii ndogo portable ambayo tunaweza tukatembea nayo ina matairi kabisa inatembea ili kuwaonesha ni namna gani tunazalisha vifaranga vya samaki aina ya sato na uzalishaji wa vifaranga vya sato huwa tunaanza na kuandaa wazazi, shughuli hiyo mara nyingi tukiwa kule Chuoni inafanyika kwenye mabwawa makubwa lakini hapa pia tumebeba tunaonesha namna gani tunaandaa wazazi”, amesema Bi. Stella.

Akielezea namna uzalishaji wa vifaranga hao unavyofanyika Bi. Stella amesema wanawaweka wazazi kwa uwiano wa dume moja na majike matatu baada ya wiki mbili wanawapokonya mayai mdomoni na kuyaweka kwenye maabara hiyo inayotembea kwenye majagi ya kuangulia ndani ya siku saba yale mayai yanakuwa yameanza kuangua na kuwa vifaranga na hivyo kuanza kuvilea vifaranga kwa siku 28 na ndipo vinapouzwa kwa mteja.

Aidha Bi. Stella amesema mbali na Maabara hiyo pia kwenye banda lao kuna samaki aina ya Sato na Kambale pamoja na samaki wa Mapambo.

“Ukija kwenye banda letu utafurahi mwenyewe tuna meza nzuri sana za kuweka sebuleni na kunakuwa na samaki wa mapambo hii inasaidia sana kwa wale watu wenye umri mkubwa kuwaondolea mawazo lakini pia vijana kuna wakati unakuta mtu umeghafirika ukiwa unawaangalia tu hawa samaki wanakusaidia kuondoa msongo wa mawazo lakini pia inapendezesha nyumba yako”, amesema Bi. Stella.

Afisa Mafunzo wa Kitengo cha Ukuzaji wa Viumbe Maji kilichopo Idara ya Shamba la Mafunzo SUA Bi. Stella Genge (Kushoto) akitoa maelezo kwa watu waliotembelea banda la Kitengo hicho. 
Mtaalamu wa Samaki kutoka SUA Bw. Elvin Vigga akiweka chakula cha vifaranga vya Samaki kwenye Maabara maalum ya kutotoreshea Vifaranga aina ya Sato. Picha zote na Nicholus Roman

Related Posts