Kongamano na Maonesho ya Kilimo 2019

kongamano na maonesho ya kilimo 2019

kongamano na maonesho ya kilimo 2019

Ndaki ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) imeandaa   Kongamano na Maonesho ya Kilimo  yatakayofanyika katika kampasi kuu ya SUA iliyopo Manispaa ya Morogoro   kuanzia Disemba 4 mpaka 6, 2019. Mada kuu ya kongamano na maonesho haya ni: Kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati na viwanda: Jukumu na michango ya wadau wa sekta za kilimo na mifugo. Tukio hili kuu litaambatana na matukio mengine madogo manne.

La kwanza litawahusisha watafiti, watunga sera na maafisa ugani kutoka wilaya zote za Tanzania. Washiriki wa mkutano huu watajadili mbinu mbalimbali za kisayansi na kisera za kutatua matatizo ya wakulima na wafugaji ili kufikia Tanzania ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Wakulima na wafugaji wakubwa kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania nao pia watapata nafasi ya kufanya kongamano lao wakati wa tukio hili. Pamoja na kujadili ufumbuzi wa matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo kwenye shughuli zao kila siku, washiriki wa kongamano hili pia watapata nafasi ya kuwasilisha mipango yao ya baadaye kwa wawekezaji na wadau wa taasisi za fedha. Aidha washiriki watapata nafasi ya kubadilishana mawazo na kushauriana na watunga sera na viongozi wa ngazi za juu wa serikali kuhusu mchango wao katika kuboresha sekta za kilimo na mifugo.

Tukio la tatu litahusisha zaidi wakulima na wafugaji wadogo na wa kati 500 kutoka wilaya zote za Tanzania watakaoshiriki kwenye mafunzo ya vitendo kwa siku tatu. Ushiriki wa wakulima na wafugaji wadogo na wa kati utawezeshwa na wadau wa maendeleo ya kilimo na mifugo vikiwemo vyama vya wakulima na wafugaji. Wakati wa mafunzo haya washiriki watapa fursa ya kujifunza mbinu za kutatua matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo katika shughuli zao za kila siku. Aidha kwa kushiriki kwenye mafunzo na maonyesho haya wakulima na wafugaji wadogo na wa kati watapata nafasi ya kuona fursa mbalimbali za kujiongezea kipato katika maeneo yao.

Kongamano hili litaambatana pia na maonesho ya wadau zaidi ya 80 wa kilimo na ufugaji. Maeneo makuu yatayopewa nafasi mwaka huu ni pamoja na: upatikanaji wa mitaji; bima za mazao; uzalishaji bora wa mazao na mifugo; kinga ya mazao na mifugo; uongezaji thamani; ufugaji nyuki na uchakataji wa asali; kilimo cha nyumba kitalu; usimamizi baada ya mavuno; nishati mbadala; umwagiliaji bora; usafirishaji wa mazao ya kilimo na mifugo; jinsi ya kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na mifugo; ufugaji wa samaki; na kilimo cha miti.

Kujisajili kama mshiriki au mwoneshaji tafadhali wasiliana na Mratibu wa tukio   Dr. John W. Massoy kupitia barua pepe tsslevents@gmail.com  au   events@tssl.co.tz    na simu 0763 300 7000754 300143  or   0714 012123.   Mwisho wa usajili wa washiriki ni Novemba 25, 2019.

Iwapo utahitaji ufafanuzi zaidi tafadhali wasiliana na   Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Prof. Sebastian Chenyambuga kupitia barua pepe    chenya@sua.ac.tz  au   chenyasw80@gmail.com  na simu   0784 754574  or 0758 23 5121.

Karibuni sana.

sign
_____________________________________
Prof. Mauild Mwatawala
MKUU WA NDAKI, NDAKI YA KILIMO

 

Downoad   PDF